Exodus 6

1 aKisha Bwana akamwambia Mose, “Sasa utaona kitu nitakachomfanyia Farao: Kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawaachia watu waende; kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.”

2 bPia Mungu akamwambia Mose, “Mimi ndimi Bwana. 3 cNilimtokea Abrahamu, Isaki na Yakobo kama Mungu Mwenyezi,
Mungu Mwenyezi hapa ni jina la Kiebrania, El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote).
ingawa sikuwajulisha Jina langu, Yehova, Mimi mwenyewe sikujitambulisha kwao.
4 ePia niliweka Agano langu nao kuwapa nchi ya Kanaani, ambako waliishi kama wageni. 5 fZaidi ya hayo, nimesikia kilio cha huzuni cha Waisraeli ambao Wamisri wamewatia utumwani, nami nimelikumbuka Agano langu.

6 g“Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi Bwana, nami nitawatoa mtoke katika kongwa la Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu. 7 hNitawatwaa mwe watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu, niliyewatoa chini ya kongwa la Wamisri. 8 iNami nitawaleta mpaka nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi Bwana.’ ”

9 jMose akawaarifu Waisraeli jambo hili, lakini hawakumsikiliza kwa sababu ya maumivu makuu ya moyoni na utumwa wa kikatili.

10Ndipo Bwana akamwambia Mose, 11 k“Nenda, mwambie Farao mfalme wa Misri awaachie Waisraeli waondoke nchini mwake.”

12 lLakini Mose akamwambia Bwana, “Ikiwa Waisraeli hawatanisikiliza, kwa nini yeye Farao anisikilize mimi, ambaye huzungumza kwa kigugumizi?”

Orodha Ya Jamaa Ya Mose Na Aroni

13 mNdipo Bwana akanena na Mose na Aroni kuhusu Waisraeli na Farao mfalme wa Misri, naye akawaamuru wawatoe Waisraeli kutoka Misri.

14 nHawa walikuwa wakuu wa jamaa zao:

Wana wa Reubeni mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli walikuwa Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi. Hawa walikuwa ndio koo za Reubeni.
15 oWana wa Simeoni walikuwa Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani. Hawa walikuwa ndio koo za Simeoni.
16 pHaya ndiyo majina ya wana wa Lawi kufuatana na orodha zao: Gershoni, Kohathi na Merari. Lawi aliishi miaka 137.
17 qWana wa Gershoni kwa koo, walikuwa Libni na Shimei.
18 rWana wa Kohathi walikuwa Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Kohathi aliishi miaka 133.
19 sWana wa Merari walikuwa Mahli na Mushi.
Hizi ndizo zilizokuwa koo za Lawi kufuatana na orodha zao.
20 tAmramu akamwoa Yokebedi, shangazi yake, ambaye alimzalia Aroni na Mose. Amramu aliishi miaka 137.
21 uWana wa Ishari walikuwa Kora, Nefegi na Zikri.
22 vWana wa Uzieli walikuwa Mishaeli, Elisafani na Sithri.
23 wAroni akamwoa Elisheba binti wa Aminadabu ndugu yake Nashoni, naye akamzalia Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari.
24 xWana wa Kora walikuwa Asiri, Elikana na Abiasafu. Hawa walikuwa ndio koo za Kora.
25 yEleazari mwana wa Aroni akamwoa mmoja wa binti za Putieli, naye akamzalia Finehasi.

Hawa walikuwa ndio wakuu wa jamaa za Walawi, ukoo kwa ukoo.

26 zHawa walikuwa Aroni na Mose wale wale ambao Bwana aliwaambia, “Watoeni Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.” 27Ndio hao hao waliozungumza na Farao mfalme wa Misri kuhusu kuwatoa Waisraeli Misri. Ilikuwa ni huyo Mose na huyo Aroni.

Aroni Kuzungumza Badala Ya Mose

28 Bwana aliponena na Mose huko Misri, 29akamwambia, “Mimi ndimi Bwana. Mwambie Farao mfalme wa Misri kila kitu nikuambiacho.”

30 aaLakini Mose akamwambia Bwana, “Kwa kuwa mimi huzungumza kwa kigugumizi, Farao atanisikiliza mimi?”

Copyright information for SwhNEN